DC Sabaya aagiza kuzimwa mwili uliozuiwa KCMC

0
204

Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya ameamuru kuzikwa kwa mwili wa mkazi wa Kijiji cha Nshara, Kata ya Machame Kaskazini, Bauda Nkya (68) baada ya mwili wake kuzuiliwa kuchukuliwa katika Hospitali ya KCMC kutokana na ndugu kushindwa kulipa gharama za matibabu zaidi ya shilingi milioni 3.5.

Nkya alifariki dunia usiku wa kuamkia Mei 2, 2021 baada ya kujikwaa kwenye kisiki mguuni na kupata jeraha lililopelekea kusababisha kifo chake.

Akizungumza mara baada ya kutembelea nyumbani kwa familia ya marehemu huyo, Sabaya amesema serikali ya wilaya itagharamia shughuli yote ya mazishi ili kuhakikisha bibi huyo anazikwa kijijini kwao.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Muro, Leonard Mbowe amesema tayari wanakijiji wamechangisha kiasi cha shilingi milioni 1.1 kwa ajili ya kulipia gharama za matibabu ili waweze kupewa mwili wao lakini uongozi wa Hospital ya KCMC uligoma kuchukuliwa kwa mwili huo hadi watakapokamilisha kulipa deni hilo.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Profesa Gileard Masenga amesema hana taarifa za kuzuiliwa kwa mwili huo kwani iwapo mgonjwa anashindwa kumudu gharama za matibabu kipo kitengo cha kufuatilia watu hao ili aweze kupewa msamaha.