Bilioni 9.5 zatengwa kujenga viwanja vitatu vya mazoezi

Michezo Tanzania

0
2227

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amesema Serikali itaanza kujenga na kukarabati viwanja vitatu vya mazoezi vya jijini Dar es Salaam, Dodoma na Geita, ambapo shilingi bilioni 9.5 zimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo kwa mwaka huu wa fedha.

Amesema zoezi hilo litaendelea kila mwaka kwa kujenga na kukarabati viwanja vya aina hiyo vitatu kwenye maeneo mbalimbali nchini, lengo likiwa ni kuibua, kukuza vipaji vya michezo na kuimarisha afya.

Dkt. Abbasi meyasema hayo wakati akifungua semina ya Waandishi wa Habari za Michezo jijini Dar es Salaam iliyoandaliwa na Bodi ya Ligi, iliyolenga kuwapiga msasa waandishi hao katika kuandika habari zenye tija kwenye tasnia ya michezo nchini.

“Kuhusu miundombinu ya michezo, mnafahamu ahadi ya serikali ya kujenga uwanja wa mpira Dodoma, utakuwa mkubwa pengine kuliko hata huu wa Mkapa, na utakuwa mkubwa Afrika Mashariki na huenda kusini mwa Bara la Afrika. Viwanja vitaendelea kujengwa hata kama sio kama huu wa Mkapa, sasa hivi tunakwenda kujenga kila mwaka viwanja vitatu vya aina ya Jakaya Kikwete Park kidongo chekundu Dar es Salaam, hivi tunavyoongea tayari tuna Bilioni 9.5 ambazo tutaanza kuboresha viwanja vya Indoor vya Dar, Dodoma na Geita,” amesema Dkt Abbasi.