Azam yaibuka na ushindi mechi dhidi ya TBC

0
240

Azam Media FC imeibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya TBC Warriors FC katika mchezo wa kirafiki uliochezwa katika Uwanja wa Shule ya Sheria (Law School of Tanzania) wilayani Ubungo mkoani Dar es Salaam.

Goli la Azam Media FC limefungwa na Contana dakika 58 ya mchezo huo uliokuwa wa kuvutia na wenye lengo la kuimarisha udugu na ushirikiano kati ya vyombo hivyo vya habari.

Baada ya mchezo huo, wachezaji na viongozi wa timu zote mbili wamezungumza machache ambapo Mwenyekiti wa Klabu ya Michezo wa TBC, Chacha Maginga amesema ni vyema taasisi zikashirikiana zaidi kwenye michezo.

“Hii mechi imeleta mahusiano mazuri, umoja na nia njema… Niwapongeze sana Azam, wana timu nzuri, wameshinda. Tutaandaa mechi ya marudiano, kwa kweli hatutakubali,” amesema Maginga.

Kwa upande wa Azam Media FC, Baruan Muhuza amesema kuwa imekuwa siku ya furaha kama walivyoahidi kwani wametimiza lengo la kuifunga TBC Warriors FC.

“Walisema masikio hayazidi kichwa lakini leo mabega yamezidi kichwa,” ameeleza Muhuza huku akisisitiza kuwa vyombo vya habari visisubiri hadi vikutanishwe na taasisi nyingine kwenye michezo, bali vinaweza kujipanga vyenyewe.