Arsenal haijaifunga Man City katika ligi tangu 2015

0
355

Arsenal inashuka dimbani leo usiku kuikaribisha Manchester City katika moja ya michezo yenye mvuto mkubwa kutokana na timu hizo mbili kuongoza kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya England (EPL).

Licha ya hilo, Arsenal inakutana na City ikikumbuka kuwa ilipoteza mchezo wa mwisho zilipokutana katika Kombe la Shirikisho (FA Cup) kwa goli 1-0, goli la Nathan Ake katika kipindi cha mbili.

Aidha, Arsenal inashuka kwenye dimba la Emirates ikiwa na kumbukumbu kuwa haijaifunga City katika mchezo wa ligi tangu ilipopata ushindi wa mwisho Desemba 2015, ikiwa ni misimu saba sasa.

Lakini la mwisho, Arsenal inashuka dimbani ikitambua kuwa endapo itapoteza mchezo wa leo, City itapanda kileleni mwa ligi, na kutia ndimu katika ndoto yake ya kutwaa ubingwa wa EPL kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 20.

Kwa hayo yote, swali litakalojibiwa baada ya dakika 90 ni, Arsena itapindua meza na kuongeza utofauti wa alama kati yake na City, au City ataendelea ubabe kwa kuifanya Arsenal kuwa kibonde?