Bingwa wa kihistoria wa ligi ya mabingwa Barani Afrika, – AL Ahly ya Misri imetinga fainali ya ligi hiyo na itamenyana na Esperance ya Tunisia kwenye mchezo wa fainali baada ya usiku wa Oktoba 23 mwaka huu timu zote mbili kusonga mbele katika michezo yao ya marudiano ya hatua ya nusu fainali.
Esperance ndio walikuwa wa kwanza kutinga fainali baada ya kupindua matokeo ya kichapo cha bao moja kwa sifuri walichokipata nchini Angola kutoka kwa wapinzani wao Premeiro Agosto.
Wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani mjini Rades, -Esperance wamewatandika Agosto mabao manne kwa mawili na kutinga fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao manne kwa matatu.
AL Ahly wao licha ya kufungwa mabao mawili kwa moja na Entente Setif ya Algeria, timu hiyo imesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao matatu kwa mawili kufuatia ushindi wa mabao mawili kwa nunge ilioupata kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza wakiwa nyumbani.
Mchezo wa kwanza wa fainali utachezwa wikiendi ya Novemba mbili au tatu, huku mchezo wa marudiano ukichezwa wikiendi itakayofuata.
Timu hizo mbili zina kumbukumbu ya kukutana kwenye fainali ya mwaka 2012 ambapo AL Ahly iliishinda Esperance.