80% kufanyia kazi nyumbani wakati wa Kombe la Dunia

0
891

Serikali ya Qatar imesema wafanyakazi wa serikali wa nchi hiyo watalazimika kufanyia kazi nyumbani wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia yatakayoanza mwezi Novemba mwaka huu nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Qatar imeeleza kuwa asilimia 80 ya nguvu kazi yake itafanyia kazi nyumbani kati ya Novemba Mosi hadi Desemba 19 mwaka huu.

Kwa upande wa shule zitapunguziwa saa za masomo wiki mbili kabla ya kuanza kwa mashindano hayo makubwa duniani na kufungwa kabisa wageni watakapoanza kuwasili nchini humo na wakati wote wa mashindano.

Qatar ni nchi ya kwanza ya Mashariki ya Kati kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia, ambapo mashindano hayo yataanza rasmi Novemba 20 mwaka huu huku fainali ikipigwa Desemba 18 mwaka huu.

Qatar inatarajia kuwa na ugeni wa takribani watu milioni 1.2, ikiwa ni karibu ya nusu ya idadi ya watu wote nchini humo.