Zoezi la uzimaji laini za simu lakamilika

0
651

Takribani miezi mitatu tangu kuanza kwa zoezi la ufungaji wa laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imemaliza zoezi hilo limekamilika kwa mafanikio makubwa.

Akizungumzia zoezi hilo Mkuu wa Mawasiliano kwa Umma wa TCRA, Fredrick Ntobi amesema kuwa jumla ya laini za simu milioni 8.7 zimezimwa baada ya muda wa usajili wa laini uliowekwa kumalizika na wahusika kutosajili laini hizo.

“Kwa kweli zoezi limefanyika kwa mafanikio, mara ya kwanza watu walidhani ni utani na walikuwa wakidai laini zetu zitazimwa, mara lugha ikabadilika ikawa laini yangu imezimwa,” alisema Ntobi.

Akizungumzia hatua inayofuata baada ya laini kufungiwa amesema ni jukumu la kampuni za mawasiliano ya simu kuhakikisha kuwa laini zote zinazotumika zimesajiliwa kwa usahihi.

Zoezi la kuzima laini za simu lilianza Januari 21 mwaka huu, baada ya Rais Dkt Magufuli kuongeza muda wa siku 20 kwa wananchi kusajili laini zao, ambapo muda wa awali ulikuwa umalizike Disemba 31, 2019.