Ziara ya Rais Magufuli nchini Zimbabwe

0
272

Rais John Magufuli ambaye amekua na ziara rasmi ya Kitaifa ya siku mbili nchini Zimbabwe, ametembelea eneo la kumbukumbu ya Mashujaa waliopigana uhuru wa Taifa hilo.

Akiwa na mwenyeji wake Rais Emmerson Mnangagwa, Rais Magufuli  ameweka shada la maua katika eneo hilo,  ambapo imezikwa miili 133 ya Mashujaa wa nchi hiyo.

Hapo jana katika mazungumzo yake na Rais Mnangagwa, Rais Magufuli amempongeza Rais huyo wa Zimbabwe kwa hatua madhubuti za kufanya mageuzi ya kiuchumi katika nchi hiyo na ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe.

Amesema katika kipindi kifupi tangu Rais Mnangagwa aingie madarakani,  hali ya uchumi imeanza kuimarika ambapo kwa sasa uchumi wa Zimbabwe unakua kwa wastani wa asilimia 3.5, mwaka ujao unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 4.2 na mwaka unaofuata kuongeza hadi wastani wa asilimi 4.4.

Kufuatia hali hiyo, Rais Magufuli ameiomba Jumuiya ya Kimataifa kuondoa vikwazo mbalimbali vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe,  kwa kuwa vikwazo hivyo vinawaumiza Raia wa nchi hiyo wakiwemo watoto na wanawake.

Kwa upande wake, Rais Mnangagwa amemshukuru Rais Magufuli kwa kukubali mwaliko wake, na amemthibitishia kuwa yeye na wananchi wa Zimbabwe wanatambua kuwa Watanzania ni ndugu zao waliojitolea kwa dhati katika ukombozi wao wakiongozwa na dhamira ya dhati ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwa kiongozi wa kwanza katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutoa msaada wa chakula, dawa na vifaa vya kujihifadhi wakati Zimbabwe ilipokumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na Kimbunga Idai mwezi Machi mwaka huu.