Zanzibar yamuaga Dkt. Magufuli

0
301

Shughuli ya kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli inaendelea katika Uwanja wa Amaan jijini Zanzibar.

Mwili huo umepelekwa Zanzibar baada ya kuagwa kitaifa hapo jana katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Akizungumza na waombolezaji katika uwanja wa Amaan, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema wakazi wote wa Zanzibar waliojitokeza kumuaga Dkt. Magufuli katika uwanja huo watapata nafasi hiyo.

Amesema baada ya kukamilika kwa shughuli ya kuaga mwili wa Dkt. Magufuli, mwili huo utalala Ikulu, ZanzIbar na utasafirishwa hapo kesho kuelekea jijini Mwanza.

Waziri Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi ya Viongozi Kitaifa amesema kuwa, kamati hiyo imejipanga vizuri ili kuhakikisha shughuli ya kuaga mwili wa Dkt. Magufuli inaenda vizuri hadi siku ya mazishi ya kiongozi huyo.

Amewashukuru Watanzania wote waliojitokeza kwa wingi kumuaga Dkt Magufuli, hali inayodhihirisha mapenzi ya dhati waliyokuwa nayo kwa kiongozi huyo.