Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC), katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwezi Novemba mwaka 2015 hadi hivi sasa, imesajili miradi 1,174 yenye thamani ya Dola Bilioni 15,756.9 za Kimarekani, huku sekta ya Viwanda ikiongoza kwa kutoa asilimia 53 ya miradi yote nchini.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Geoffrey Mwambe, alipokua akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka minne, chini ya uongozi wa Rais John Magufuli.
Ameongeza kuwa, kati ya miradi yote iliyosajiliwa nchini, sekta ya Viwanda ina jumla ya miradi 626, huku miradi yenye uwekezaji mkubwa ikiendelea kuwavutia Wawekezaji na kuzidi kuajiri maelfu ya Watanzania.
Mwambe amesema kuwa, kupitia miradi hiyo iliyosajiliwa nchini, zaidi ya ajira Laki Moja na Nusu za moja kwa moja zimezalishwa na nyingine 60,465 zimezalishwa kutokana na ukuaji Sekta wa Viwanda nchini.
‘’Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuongeza masoko ya bidhaa zetu za ndani, na tangu dhamira ya uchumi wa viwanda itangazwe tumeshuhudia ujenzi wa viwanda vingi ikiwemo viwanda vya maziwa katika maeneo mbalimbali ya nchi, na sasa hatuagizi maziwa kutoka Uholanzi na jirani zetu nchi ya Kenya kama tulivyokuwa tukifanya huko nyuma’’ amesema Mwambe.
Kwa mujibu wa Mwambe, TIC imeendelea kuimarisha mifumo na taratibu mbalimbali za uwekezaji nchini ambazo awali zilikuwa zikileta usumbufu na vikwazo kwa Wawekezaji, ambapo kwa sasa imeongeza Watumishi ili kurahisisha upatikanaji wa leseni na vibali mbalimbali.
Akitolea mfano amesema kuwa, kabla Serikali ya awamu ya Tano haijaingia madarakani, TIC ilikuwa na Watumishi Watano kutoka katika Idara mbalimbali za Serikali, lakini kwa sasa kuna jumla ya Watumishi 25 kutoka Wizara, Idara, Wakala na Taasisi mbalimbali za Serikali.
“TIC tumewaweka pamoja Watumishi wa Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Umma kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa leseni na vibali, na sasa kuna huduma zote za msingi kwa Mwekezaji zinazotolewa moja kwa moja katika dawati letu” amesema Mwambe.
