WWF yaunga mkono urejeshaji uoto wa asili

0
217

Takwimu za mwaka 2017 zinaonyesha kuwa zaidi ya hekta laki nne na elfu sitini za misitu Tanzania hupotea kila mwaka, kutokana na uharibifu wa mazingira na ukataji hovyo wa misitu.

Hayo yameelezwa na meneja wa Uhifadhi kutoka Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) Dkt. Lawrence Mbwambo wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari wa mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar es Salaam yanayofanyika wilayani Kilwa.

Lengo la mafunzo hayo ni kujenga uelewa wa pamoja juu ya uhifadhi wa mazingira hasa kupitia dhana ya urejeshaji wa uoto wa asili kwenye maeneo ambayo yameathirika zaidi na uchafuzi wa mazingira.

Aidha Dkt. Mbwambo amesema kwa mujibu wa takwimu za miaka mitano iliyopita, kwa Afrika pekee hekta milioni 3.9 hupotea kila mwaka ambapo kwa dunia jumla ya hekta milioni saba hupotea.

Amesema WWF inaunga mkono juhudi za serikali za kurejesha uoto wa asili katika maeneo yaliyoharibiwa ambayo ni takribani hekta milioni 5 2 ifikapo mwaka 2030.