Wizara ya Maliasili yaomba bilioni 620

0
119

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Pindi Chana leo amewasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 ya zaidi ya shilingi bilioni 620.

Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jijini Dodoma Balozi Chana amesema kati ya fedha hizo zaidi ya shilingi bilioni 443 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na zaidi ya shilingi bilioni 180 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Ameongeza kuwa sekta ya utalii hasa utalii wa ndani nchini umeendelea kukua kutokana uhamasishaji ambao umekuwa ukifanyika.

“Wizara imeendelea kuhamasisha utalii wa ndani kupitia kampeni na programu mbalimbali, hatua hizi zimeongeza idadi ya watalii wa ndani waliotembelea maeneo ya hifadhi, vituo vya malikale na makumbusho kutoka watalii 562,549 mwaka 2020 hadi 788,933 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 40.2.” amesema Balozii Chana

Kwa mujibu wa waziri huyo wa Maliasili na Utalii, Tanzania imeendelea kutambulika kimataifa baada ya kupata tuzo mbalimbali ikiwemo ile ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kuwa hifadhi inayoongoza kwa ubora Barani Afrika kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021.