Wizara ya Maji yaagizwa kuongeza kasi ya miradi

0
152

Wizara ya Maji imeagizwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji na kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema hatua hiyo itaiwezesha serikali ifikapo mwaka 2025 ifikie lengo lake la kufikisha huduma ya maji safi na salama kwa wananchi kwa wastani wa asilimia 85 maeneo ya vijijini na asilimia 95 maeneo ya mijini na hivyo kuwaondolea wananchi adha ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Dkt. Mpango ametoa agizo hilo kwa Waziri wa Maji Jumaa Aweso, alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa nane wa mwaka wa Bodi za Maji za Mabonde, unaofanyika jijini Mbeya.

Aidha Dkt. Mpango amewaagiza wakuu wa mikoa yote nchini kulinda vyanzo vya maji vilivyopo katika maeneo yao, kuwaondoa wote waliojenga katika maeneo ya vyanzo vya maji na kuwatafutia maeneo mbadala pamoja na kuendeleza zoezi la upandaji miti rafiki wa maji katika mikoa yao ili kuendelea kulinda vyanzo vya maji vilivyopo.

Pia Makamu wa Rais amewataka washiriki wa
mkutano huo mkuu wa nane wa mwaka wa Bodi za Maji za Mabonde kujadili njia za kukabiliana mabadiliko ya Tabianchi na kulinda vyanzo vya maji.