Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe amevitaka vyombo ya habari vya nchi za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania, kutangaza na kuandika habari za kweli ili kujitofautisha na vyombo vya habari vya nje ambavyo vimekua vikipotosha na kubeza kwa makusudi mambo mazuri yanayotekelezwa na yaliyotekelezwa na nchi za Afrika.

Akizungumza jijini Dar es salaam wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya mawasiliano Barani Afrika, Dkt Mwakyembe amesema kuwa vyombo vya habari vya Afrika havina budi kuonyesha udhubuti kwa kuweka sera zinazoakisi maendeleo na kuyatangaza kwa Wananchi wake na wote waliopo nje ya Bara hilo.
Dkt Mwakyembe amefafanua kuwa sehemu kubwa ya maudhui ya vyombo vya habari vilivyopo nje ya Bara la Afrika, hayaonyeshi nchi za Afrika zinavyopiga hatua za maendeleo kwa wananchi wake na badala yake hupenda kuripoti na kutangaza mambo mabaya ikiwa ni pamoja na njaa, magonjwa, vurugu za kisiasa na vita.
Amewataka vijana wa nchi za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania, kujifunza historia ya Bara lao ili waweze kufahamu wapi walipotoka na wapi wanapoelekea badala ya kupenda kulalamika pasipo na kuweka mikakati ya namna bora ya kupiga hatua za kujietea maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi amesema kuwa, serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za mawasiliano katika sekta binafsi, ili kuhakikisha kuwa wanajenga daraja moja katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya sekta ya habari na mawasiliano nchini.
