WFP yawashika bega wakulima

0
93

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeipatia wizara ya Kilimo ndege nyuki (drone) na vishkwambi 370 kwa ajili ya kusaidia shughuli za kilimo nchini.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo jijini Dodoma, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema vifaa hivyo vitasaidia kukabiliana na uharibifu wa mazao shambani na kusaidia kilimo kuwa na tija katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema ndege nyuki aliyopokea ina uwezo wa kupulizia dawa na viuatilifu katika hekta 20 huku vishkwambi 370 vyenye thamani ya
shilingi Milioni 364 vitarahisisha utekelezaji wa dhana ya kilimo ni sayansi kwa kutatua changamoto za Wakulima kupitia teknolojia.

“Nawashukuru sana WFP kwa kutupatia vifaa hivi, ambapo vishkwambi vinakwenda kugawiwa kwa Maafisa Ugani kwa ajili ya kukusanya taarifa mbalimbali za Kilimo,” amesema Waziri Bashe.

Ameeleza kuwa vifaa hivyo vitaanza kutumika kwa kupima mashamba ya vijana wa programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT).

Naye Mwakilishi Mkazi wa WFP, Sarah Gibson ameeleza kufurahishwa na ushirikiano aliopewa na wizara ya Kilimo na kuahidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania ili kukuza sekta ya kilimo.