Wezi wa tani tano za nondo Mbaroni

0
502

Agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa latendewa kazi

Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro, limewakamata watu watano kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa tani tano za nondo zilizokua zikitumika kwenye mradi wa ujenzi wa stendi kubwa ya mabasi ya Kimataifa ya Moshi.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kilimanjaro, -Hamisi Issah amethibitisha kukamatwa kwa watu hao akiwemo Daudi Audifasi mkazi wa eneo la RAU,  ambaye anadaiwa kutoboa uzio wa stendi hiyo kwa chini, na kukutwa na nondo nyumbani kwake ambako ni mita kumi kutoka eneo la tukio.

Ameongeza kuwa nondo hizo zilizoibwa  katika tukio lililotokea tarehe Sita mwezi huu, nazo zimekamatwa na ziko polisi.

Hatua ya kukamatwa kwa Watu hao watano wanaotuhumiwa kuhusika na wizi wa tani tano za nondo zilizokua zikitumika kwenye mradi wa ujenzi wa stendi kubwa ya mabasi ya Kimataifa ya Moshi, inafuatia agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye anaendelea na ziara yake ya siku Nne mkoani Kilimanjaro.

Akitoa agizo hilo, Waziri Mkuu Majaliwa, alimtaka Kamanda huyo wa  polisi wa mkoa wa Kilimanjaro, -Hamisi Issah kuhakikisha anawasaka na kuwafikisha katika vyombo husika, watu wanaotuhumiwa kuiba nondo  hizo na kisha kutoroka.

Ujenzi wa stendi hiyo kubwa ya mabasi ya Kimataifa ya Moshi,  unafanywa na Mkandarasi Mkuu ambaye ni kampuni ya CRJE ya nchini China, akishirikiana na Wakandarasi Wasaidizi watano na unatarajiwa kukamilika mwezi Januari mwaka  2021,  kwa gharama ya Shilingi Bilioni 28 Nukta Nane.