Wenye viwanda wapatiwa taaluma ya KAIZEN

0
142

Katibu Mkuu wa wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amewaomba wamiliki wa viwanda nchini kutumia taaluma ya KAIZEN, kuunga mkono juhudi za Serikali kufungamanisha uchumi kupitia sekta za viwanda na biashara ili kuleta matokeo chanya ya Taifa.

Dkt. Hashil
ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati akizungumza na wakufunzi na wenye viwanda wanaotekeleza taaluma ya KAIZEN.

Amesema utekelezaji wa KAIZEN katika sekta ya viwanda umewezesha kuandaliwa kwa takribani waratibu 200 wa taaluma hiyo kutoka viwandani na wakufunzi 300 ambapo 175 wamepatiwa vyeti na tayari wakufunzi 84 wamesajiliwa.

Katibu Mkuu huyo wa wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara amesema lengo ni kuyafikia maeneo mengi kisekta kwa haraka mijini
na vijijini. 

Hadi sasa, zaidi ya viwanda 130 vimenufaika na mafunzo ya KAIZEN.

Kwa upande wake Balozi wa Japan nchini Yasushi Misawa amekipongeza kiwanda cha A – Z kilichopo mkoani Arusha kwa kutekeleza taaluma ya KAIZEN na kuibuka mshindi katika mashindano ya KAIZEN Africa yaliyofanyika nchini Tunisia.