Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu akitoa taarifa ya matumizi ya Fedha za Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO – 19.
Akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa vyumba vya madarasa katika mikoa yote 26 hapa nchini, Waziri Ummy amesema mpaka sasa ujenzi huo umefikia asilimi 95 na kwamba majiji matatu ya Arusha, Mwanza na Mbeya yameongezewa muda kutokana na ujenzi wa madarasa katika maeneo hayo kuwa ni ghorofa.
Mbali na shule, waziri Ummy amesema fedha nyingine zinakwenda kujenga vituo vya afya 233 nchi nzima, ili kuondoa tatizo la upatikanaji wa huduma za afya kwenye maeneo mengi hapa nchini.
Ameongeza kuwa fedha za tozo za miamala ya simu zaidi ya shilingi bilioni saba zimepelekwa kumalizia maboma ya madarasa zaidi ya 500 kwenye maeneo mbalimbali, huku akisema mahitaji ni makubwa kulinganisha na fedha zinazotolewa.
Kuhusu Miundombinu ya barabara ambayo inasimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Serikali imepeleka jumla ya shilingi bilioni 330.47 kutoka katika tozo na tayari Wakala huo umesaini mikataba na Wakandarasi mbalimbali katika kila halmashauri ili kujenga barabara za wilaya na maeneo ya vijijini.