Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga tarehe 29 Julai 2019 amewasili Mkoani Simiyu kwa ajili ya kujionea maandalizi ya Maadhimisho ya 26 ya sikukuu ya wakulima maarufu kama (Nane Nane) yenye lengo la kuwatambua na kuwaenzi Wadau Wakuu wa Sekta ya Kilimo hapa nchini.
Sekta ambazo zinashirikishwa katika maadhimisho hayo ni kilmo, Wafugaji, Wavuvi, Wanaushirika, Wasindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili kwa mchango wao mkubwa wanaoutoa katika kuendeleza uchumi wa nchi yetu.
Mwaka huu wa 2019, sherehe hizi zinafanyika Kitaifa mjini Bariadi katika Viwanja vya maonesho ya kilimo Nyakabindi katika Mkoa wa Simiyu hivyo Mhe Hasunga amepongeza Uongozi wa mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara kwa juhudi zao za kufanikisha kuingiza uwanjani huduma za msingi ambazo ni maji na umeme.
Amesema kuwa jukumu hilo kwa Serikali na Wadau
wa Sekta Binafsi ni kuendeleza viwanja hivyo vya Nyakabindi kwa kujenga mabanda
ya maonesho ya kudumu na kuboresha huduma muhimu za kijamii ili kuwe na
maonesho endelevu yenye sura ya Kitaifa na Kimataifa.
Amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali, imeendelea kuongeza na kuboresha viwanja vya maonesho katika Kanda mbalimbali hapa nchini, kwa sasa kuna viwanja nane (8) vya maonesho ya kilimo ambavyo ni Themi (Arusha) Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara; Mwl. J.K.Nyerere (Morogoro) Kanda ya Mashariki ambayo mikoa yake ni Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Tanga;na John Mwakangale (Mbeya) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inayojumuisha mikoa ya Iringa, Mbeya, Ruvuma, Njombe, Katavi, Songwe na Rukwa;
Vingine ni Nzuguni (Dodoma) katika Kanda ya Kati yenye mikoa ya Dodoma na Singida; Nyakabindi (Bariadi) Kanda ya Ziwa Mashariki yenye mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara; Nyamuhongolo (Mwanza) Kanda ya Ziwa Magharibi yenye mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita; Ngongo (Lindi) Kanda ya Kusini inayojumuisha mikoa ya Mtwara na Lindi na Fatma Mwasa (Tabora) Kanda ya Magharibi yenye mikoa ya Tabora na Kigoma.
Akizungumza na mtandao wa Wazo Huru Blog, Waziri huyo wa kilimo ameeleza kuwa Wakati wa sherehe hizo za Nane Nane, Wakulima, Wafugaji, Wavuvi, Wanaushirika na Wadau wengine katika Sekta za Kilimo; watapata fursa nzuri zaidi ya kuona na kujifunza mbinu na teknolojia sahihi za uzalishaji na usindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, maliasili na bidhaa nyinginezo kupitia Maonyesho ya Kilimo yanayoandaliwa.
Aidha, kwa Wafanyabiashara itakuwa ni fursa nzuri ya kutangaza bidhaa zao
hususani pembejeo na zana mbalimbali za uzalishaji na usindikaji wa mazao ya
kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili.
Aliitaja Kaulimbiu ya sherehe za Nane Nane Mwaka huu ni kuwa ni “Kilimo, Mifugo
na Uvuvi kwa ukuaji wa Uchumi wa Nchi”. Kaulimbiu hii imechaguliwa baada
ya kutafakari kwa undani suala zima la Uchumi wa Viwanda unavyoweza kuchangia
katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, pato la Taifa na wakati huo huo
kupambana na Umaskini.
“Ni ukweli ulio dhahili kuwa Kilimo ni Sekta kubwa na muhimu kwa maendeleo kutokana na mchango wake katika uchumi wa Taifa. Mfano katika mwaka 2017, Sekta ya Kilimo ilitoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 65.5, ikichangia asilimia 28.7 ya pato la Taifa. Sambamba na hilo Sekta ya Kilimo inachangia asilimia 65 ya malighafi za viwandani. Takwimu zinaonesha kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2018 ukuaji wa Sekta ya Kilimo ulifikia asilimia 7.1” Alikaririwa Mhe Hasunga
Ameongeza kuwa Kaulimbiu ya mwaka huu inahamasisha Wakulima, Wafugaji, Wavuvi
na Wanaushirika kuleta mapinduzi katika Sekta za Kilimo kwa kuzalisha kwa tija
ili kukuza uchumi wa Mkulima, Mfugaji, Mvuvi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Kadhalika, ametoa wito kwa Wananchi na Wadau wote
kushiriki kikamilifu na kuhudhuria kwa wingi maonesho hayo kuanzia tarehe 1
hadi 8 Agosti, 2019