Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kirusi kipya cha UVIKO – 19 ambacho tayari kimeingia katika nchi mbalimbali zikiwemo za Afrika, bado hakijafika nchini.
Waziri Ummy ametoa kauli hiyo mkoani Dar es Salaam wakati akipokea chanjo dhidi ya UVIKO – 19 aina ya Sinovac kutoka nchini Uturuki na kuongeza kuwa, taarifa alizopata hadi leo asubuhi ni kuwa kirusi kilichopo nchini ni Omicron pekee.
Amefafanua kuwa leo asubuhi amefanya mawasiliano na maafisa wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu kirusi hicho kipya na wamemueleza kuwa bado wanaendelea kufanya tafiti kujua kitakuwa kikali kiasi gani na madhara yake yatakuwaje.
Kwa mujibu wa Waziri Ummy, sampuli alizoelekeza zichukuliwe kuangalia kama Tanzania ina kirusi hicho kipya cha UVIKO – 19 zimeonesha bado kuna Omicron pekee.