Serikali ina mpango wa kuwa na kituo kimoja cha kulipia tozo zote za mazao ya mifugo na uvuvi, pamoja na kuondoa tozo ambazo zinakwamisha sekta hizo zisikue.
Mpango huo umetangazwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki wakati akizungumza na baadhi ya Wavuvi katika kata ya Nyamikoma wilayani Busega mkoani Simiyu, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku moja mkoani humo.
Amesema wizara ya Mifugo na Uvuvi itaangalia tozo ambazo zitakuwa rafiki kwa Wawekezaji, Wafanyabiashara, Wafugaji na Wavuvi wa hali ya chini ili kuhakikisha sekta za mifugo na uvuvi zinachangia kwa sehemu kubwa pato la Taifa.
“Tutaenda kuangalia ni tozo zipi na baadhi tayari mmeshazitaja zikiwemo za kusafirisha mazao ya mifugo na uvuvi nje ya nchi halafu tunatafuta namna ya kuwa na kituo kimoja cha kulipia hizi tozo zote,” amesema Waziri Ndaki.
Akiwa amefuatana na Naibu Waziri wa wizara hiyo Pauline Gekul katika ziara yake, Waziri Ndaki ameongeza kuwa uwepo wa tozo ambazo zitakuwa rafiki katika kukuza sekta za Mifugo na Uvuvi kutasababisha watu wengi kuwekeza katika sekta hizo na kukuza pato la Taifa kwa kuwa shughuli za kuchumi zitaongezeka.
Kwa upande wake Naibu Waziri Gekul ameendelea kuwasisitiza watu wanaondelea kujihusisha na uvuvi haramu kuacha mara moja vitendo hivyo, kwa kuwa wizara haitawafumbia macho watu ambao bado hawataki kuacha kuharibu mazao ya uvuvi.
Amesema ni wakati sasa jamii kushirikiana na Serikali kuwabaini watu wanaojihusisha na uvuvi haramu, kwa kuwa wanaishi katika maeneo wanayofahamika ili Serikali ichukue hatua na kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi itazidi kutoa elimu kwa jamii juu ya athari za uvuvi haramu.