Waziri Ndaki azindua mfumo wa ukaguzi wa mifugo

0
177

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amezindua mfumo wa ukaguzi wa mifugo na mazao yake na kuwataka watakaotekeleza mfumo huo kuto wanyanyasa wananchi.

Waziri Ndaki ametoa kauli hiyo jijini Dodoma, wakati wa uzinduzi wa mfumo huo ili kuongeza tija na kuinua pato la taifa kupitia sekta ya mifugo.

Amesema mfumo huo ni rahisi na ushirikishwaji hivyo ni vyema wakaguzi kutogeuka kuwa Jeshi la Polisi na kuwasumbua wadau wa sekta ya mifungo.

“Utaratibu huu ni wa ushirikishwaji, sasa tunapokuwa huko kufanya ukaguzi kuhusiana na ubora na viwango tusijigeuze sisi kuwa polisi. Kwa nchi yetu mfumo huu ni rahisi na ambao umelenga kuzipatia taarifa wizara, taasisi na wadau wengine kuhusiana na ukaguzi, ubora na usalama wa mifugo pamoja na mazao yake.” Amesema Ndaki

Ameongeza kuwa umuhimu wa mfumo huo ni kuhakikisha utekelezaji wa wajibu wa kulinda afya za walaji, mifugo na mazao yake kwa kusimamia sheria, kanuni na taratibu jambo ambalo litasaidia wafugaji kuzalisha mifugo kwa tija kwa kutumia pembejeo na huduma zilizosajiliwa na kutambuliwa kisheria.

Aidha ametoa rai kwa wakaguzi kutumia mfumo wa ukaguzi wa mifugo na mazao yake kuhakikisha sheria, kanuni, taratibu za kusimamia na udhibiti wa ubora, usalama na viwango stahiki vinasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo.

Pia, ametumia fursa hiyo, kutoa wito kwa wataalam wa wizara, mamlaka za serikali za mitaa, taasisi na wadau waliopo kwenye vyama vya tasnia kuhakikisha wakaguzi, wazalishaji, watoa huduma kwenye mifugo wanazingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo ili kuhakikisha mlaji wa mifugo na mazao yake anaendelea kunufaika kiafya na kimaslahi kupitia maziwa, nyama na mayai na bidhaa nyingine.