Waziri Ndaki asisitiza Wafugaji kuwa na ng’ombe bora

0
144

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amewashauri Wafugaji nchini kufikiria kuwa na ng’ombe bora badala ya kuwa na ng’ombe wengi wasio na ubora, ambao hawakidhi tija katika maisha yao kwa kutotoa mazao bora.

Waziri Ndaki ametoa ushauri huo katika kijiji cha Kinango kilichopo wilaya ya Magu mkoani Mwanza wakati akishuhudia zoezi la uogeshaji mifugo dhidi ya magonjwa mbalimbali wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani humo.

Amesema mifugo mingi wakiwemo ng’ombe, ni njia mojawapo ya kutunza fedha ambayo imekuwa ikitumiwa na Wafugaji, hivyo ni muhimu Wafugaji wakahakikisha mifugo yao inakuwa bora kwa kuipatia huduma muhimu ikiwemo ya kuiogesha.

“Nchi yetu tuna ng’ombe wengi sana, lakini wengi siyo bora kama inavyotakiwa, sasa tunatakiwa kutoka kuwa na ng’ombe wengi tu bali tuwe na ng’ombe walio bora, tukiwa na ng’ombe wengi wasio bora hawatusaidii sana katika maisha yetu kwa sababu lengo la kuwa na ng’ombe atupe nyama, atupe maziwa na atupe kipato sasa tufikirie kuwa na ng’ombe bora na moja ya njia ya kuwa na ng’ombe bora ni hii ya kuwaogesha,” amesema Waziri Ndaki.

Ameongeza kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetenga bajeti ya kukarabati majosho kadhaa yaliyopo kwenye  maeneo mbalimbali nchini na kwamba majosho matano yaliyopo katika wilaya ya Magu nayo yatakarabatiwa ili mifugo mingi iweze kuogeshwa na kuwa bora.

Waziri Ndaki akiwa ameongozana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Pauline Gekul katika ziara hiyo amesema kuwa, njia nyingine ya kuwa na ng’ombe bora ni Wafugaji kuhakikisha mifugo yao inapata malisho bora ambayo yatafanya mifugo hiyo kuwa na afya bora.

Kwa upande wake Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Nchini (TMB) Iman Sichalwe amewaeleza Wafugaji kuwa suala la kuogesha mifugo dhidi ya magonjwa ni muhimu, kwa kuwa Tanzania imekuwa ikishindwa kuuza nyama katika nchi mbalimbali kutokana na viwanda vya kuchinja na kuchakata nyama kutopata mifugo bora.