Waziri Nape : Uchumi wa vyombo vya habari hauridhishi

0
147

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema, anafahamu hali ya uchumi wa vyombo vya habari nchini si nzuri.

Amesema hata magazeti yaliyofunguliwa Februari 10 mwaka 2022 ambayo ni Mwanahalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima bado hayajaanza kuchapishwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na pia kuna madeni ambayo vyombo vya habari vinadai na bado hayajalipwa.

Waziri Nape ameyasema hayo mkoani Morogoro wakati akifungua mkutano mkuu wa 12 wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF) na kuongeza kuwa Serikali inafahamu kuhusu changamoto hiyo.

“Kutokana na hali ya uchumi usioridhisha katika vyombo vyetu vya habari, mwezi Januari mwaka huu niliunda Kamati Maalum ya kufanya Tathmini ya Hali ya Uchumi wa vyombo vya Habari inayoongozwa na Mwenyekiti kaka yangu Tido Mhando na ndugu yangu Bakari Machumu yumo kwenye Kamati hii. Sasa Kamati hii inaendelea kufanya kazi yake na itakuja na mapendekezo ya nanma ya nini kifanyike ili kukwamua uchumi katika Vyombo vyetu vya Habari.” amesema Waziri Nape

Aidha, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ana dhamira ya dhati katika kuimarisha sekta ya habari, ambapo juhudi kubwa alizozifanya kwa sekta hiyo tangu aingine madarakani ni kuzipitia sheria zinzolalamikiwa na wadau ikiwemo ile ya Huduma za Habari Namba 12 ya mwaka 2016.

Wakati wa mkutano mkuu huo wa 12 wa Jukwaa la Wahariri nchini, Waziri Nape amepokea tuzo ya kutambua mchango wake wa kuendelea kujitolea kuboresha mazingira ya kazi ya vyombo vya habari nchini kutoka kwa Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile.