Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema maagizo na maelekezo yote ambayo yametolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka kwa Mkoa wa Lindi yatatekelezwa na watumishi wote wa umma.
Akizungumza katika mkutano wa majumuisho ya ziara ya Shaka mkoani Lindi, ulioifanyika katika Chuo cha Ualimu Nachingwea, Waziri Mkuu amesema yote ambayo yameelezwa yatafanyiwa kazi na hakuna hata agizo moja ambalo hatatekelezwa.
“Umekutana na wananchi wa Mkoa wa Lindi, umetembelea miradi ya maendeleo, sisi wana Lindi tumefurahi sana kupata taarifa yako ya mafanikio ambayo yamepatikana, umewapongeza watumishi wa umma, nataka kukuhakikishia nami nilifanya ziara kwenye Halmashauri zote za mkoa huu.
“Ulichokiona wewe nami ndicho nilichokiona watumishi hawa ndio wanaotekeleza miradi hiyo. Mkoa wa Lindi kuna mabadiliko na hizi ni jitihada zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi kupitia Serikali yetu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Waziri Mkuu.
Awali akizungumza wakati wa majumuisho hayo, Shaka ameeleza kwa kina kuhusu mafanikio ambayo ameyashuhudia kwenye Mkoa wa Lindi na hiyo yametokana na upendo mkubwa alionao Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa Lindi na Watanzania kwa ujumla.
“Katika Mkoa wa Lindi nimepita kila mahali kunajengwa, barabara zinajengwa, vituo vya afya, shule na majengo mengine ya huduma za kijamii yanaendelea kujengwa, Serikali imetoa zaidi ya Shilingi bilioni 52 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo,” amesema Shaka.