Waziri Mkuu : Tunahitaji Watumishi waadilifu

0
175

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa, Serikali inahitaji Watumishi waadilifu, wenye uwezo wa kufanyakazi kwa uaminifu na walio tayari kuwahudumia Wananchi wote bila ya ubaguzi.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo mkoani Iringa, wakati akizungumza na Watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mufindi, Halmashauri ya Mji wa Mafinga pamoja na Madiwani, kwenye mkutano uliofanyika katika halmashauri ya Mufindi.

Amesema kuwa, Serikali inataka kuona Watumishi wa umma wakitumia taaluma zao katika kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili Wananchi kwenye maeneo yao hasa ya vijijini, na hivyo kuwataka watenge muda wa siku Nne kwa ajili ya kukutana nao.

“Tuelewane vizuri hapa, msimamo wa Serikali hii ni kuchapakazi, mtu atakayevurugavuruga hana nafasi katika Serikali hii, na hatutamuundia Tume tutamalizana naye hapo hapo, Rais wetu anataka kuona Wananchi wakihudumiwa katika maeneo yao”, amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Pia amezikumbusha halmashauri zote nchini, zihakikishe zinatenga asilimia Kumi ya mapato yake kwa ajili ya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu.

Naye Mkuu wa mkoa wa Iringa, – Ally Happi amesema kuwa, halmashauri za wilaya ya Mufindi na Halmashauri ya Mji wa Mafinga zinafanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato, pamoja na kutenga asilimia Kumi ya mapato yake kwa ajili ya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu.

Akizungumzia changamoto inayoikabili hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Happi amesema kuwa hospitali hiyo imekua ikihudumia halmashauri mbili ambazo ni Mufindi na Mafinga, lakini mgawo wa dawa unaopelekwa ni kwa ajili ya wakazi wa Mafinga pekee.