Waziri Mkuu Majaliwa kuhudhuria mkutano wa NAM

0
277

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, leo anamwakilisha Rais John Magufuli katika mkutano wa 18 wa Wakuu wa nchi na Serikali wa Nchi zisizofungamana na upande wowote (NAM) kutoka Afrika na Mataifa mengine Duniani, mkutano unaofanyika huko Baku, – Azerbaijan.
 
Mkutano huo unalenga kujadili namna ya kutatua changamoto za Kisiasa, Kiuchumi na Kijamii zinazozikabili nchi Wanachama wa NAM.
 
Ajenda za mkutano huo ni kupokea ripoti za mkutano wa maandalizi wa Mawaziri, kupokea ripoti ya mkutano wa maandalizi wa Maafisa Waandamizi na uchaguzi wa nchi zitakazokuwa Wajumbe katika ofisi ya uratibu wa shughuli za NAM huko New York,- Marekani kwa kipindi cha mwaka 2019 hadi mwaka 2022.
 
Waziri Mkuu Majaliwa anahudhuria mkutano huo wa 18 wa Wakuu wa nchi na Serikali wa Nchi zisizofungamana na upande wowote akiwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Damas Ndumbaro na Balozi wa Tanzania katika nchi za Russia na Azerbaijan,- Meja Jenerali Mstaafu Simon Mumwi. 
 
Kabla ya kwenda Azerbaijan, Waziri Mkuu Majaliwa alikuwa Sochi nchini Russia ambako pia alimwakilisha Rais Magufuli katika mkutano kati ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Afrika pamoja na Russia.