Waziri Mkuu Majaliwa amlilia mfanyabiashara Subhash Patel

0
151

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya Motisun Group, – Subhash Patel kilichotokea jijini Dar es salaam.
  
Katika salamu zake Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa  amehuzunishwa na kifo cha mfanyabiashara huyo maarufu nchini, ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI) na mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
 
Patel amefariki dunia nyumbani kwake Kisutu jijini Dar es salaam ambako alikuwa akiendelea na matibabu na anatarajiwa kuzikwa keshokutwa Alhamisi kwenye makaburi ya Wahindu yaliyoko Kijitonyama jijini Dar es salaam.
 
Mfanyabiashara huyo maarufu nchini alikuwa akimiliki kampuni zinazotengeneza bidhaa za plastiki, saruji, bati, nondo, nyaya za umeme, vinywaji, rangi na pia alimiliki hoteli za White Sands, Sea Cliff na Pearlsun Hotel & Resorts.