Waziri Mkuu : Dodoma inaendelea kujengwa

0
199

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewatoa hofu Watanzania kuhusu kuendelezwa kwa Makao Makuu ya nchi Dodoma kwa kusema kuwa, Serikali imeweka mfumo mzuri utakaohakikisha yanajengwa kuendana na mipango ya maendeleo ya jiji la Dodoma.
 
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022
 
Amesema mfumo huo unahusisha kikosi kazi cha Taifa cha kuratibu mpango wa Serikali wa kuhamia Dodoma, ambacho kinajumuisha wajumbe kutoka wizara na taasisi za Serikali.

“Kikosi kazi hicho kina jukumu la kushauri namna bora ya kupanga na kuendeleza mji wa Serikali na jiji la Dodoma kwa ujumla,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
 
Amesema utekelezaji huo unahusisha miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na maji, uwanja cha ndege, barabara na utoaji wa huduma za jamii.
 
Wakati huohuo Waziri Mkuu Majaliwa ametoa wito kwa wabunge na Watanzania wote kukumbuka kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwataka waendelee kushikaman na kuwa wamoja kama Taifa.
 
“Huu si wakati wa kunyoosheana vidole bali ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele, kwa msingi huo tuendelee kudumisha na kuilinda amani ya nchi yetu ikiwa ni sehemu ya kuenzi jitihada za waasisi wa Taifa hili,” amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.