Waziri Mkuu azindua mpango wa tatu wa maendeleo wa Taifa

0
146

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano kuanzia 2021/22 hadi 2025/2026 jijini Dodoma

Akizindua mpango huo amesema mpango wa kwanza na wa pili umesaidia katika ukuaji wa maendeleo ya watu na Taifa ikiwepo katika sekta ya elimu, barabara, afya, kilimo na sekta nyingine nyingi

Aidha, Majaliwa amesema katika mpango wa pili wa maendeleo, kwenye sekta ya elimu Serikali imesimamia kutoa elimu bila malipo shule za msingi na sekondari, kuongeza mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kuendelea kujenga vyuo vya ufundi na ufundi stadi nchini, kuongeza ujuzi na kuwawezesha vijana kujiajili

“Tumeendelea na ujezi wa hospitali za kanda, hospitali za mikoa, hospitali za wilaya, vituo vya afya pamoja na zahanati ili kufikisha huduma za afya karibu na wananchi hivyo kupunguza maradhi na vifo hususani mama wajawazito na watoto walioko chini ya umri wa miaka mitano,” ameeleza Waziri Mkuu

Kwa upande wake mwakilishi wa sekta binafsi amesema sekta binafsi zimeshirikishwa kikamilifu katika mipango yote iliyopita na anatarajia katika mpango huu wa tatu watashiriki katika kuimarisha uchumi ili kuiwezesha nchi kuingia uchumi wa kati ngazi ya juu.

Dira ya Taifa ya maendeleo 2025 inalenga Tanzania kufikia nchi yenye hadhi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025, ikiwa na sifa za maisha bora na mazuri, amani, utulivu na umoja, utawala na uongozi bora, jamii iliyoelimika na inayopenda kujifunza na uchumi wenye uwezo wa ushindani na kujiletea ukuaji wa maendeleo ya watu.