Waziri Mkuu aunda Kamati maalum kuchunguza mauaji Mtwara

0
124

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameunda timu maalum ya watu tisa ambayo imepewa jukumu la kuchunguza mauaji yaliyofanyika Mtwara na Kilindi, Tanga.

“Kamati hiyo inapaswa kuanza kazi yake kesho na inatakiwa iwe imekamilisha ripoti yake ndani ya siku 14,” amesema Waziri Mkuu ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa leo Ijumaa, Februari 4, 2022 wilayani Magu, Mwanza akiwa njiani kuelekea Musoma, Mara kwenye maadhimisho ya miaka 45 ya CCM.

Rais Samia amesema anatambua Jeshi la Polisi limeunda kamati ya uchunguzi lakini ameagiza iundwe kamati hiyo huru ili ikafanye uchunguzi wa mauaji ya Mtwara yaliyofanywa na askari polisi.

Mauaji ya Mtwara yalitokea Januari 05, 2022 na mauaji ya Kilindi yaliyotokea Januari 30, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Kamati hiyo ina maafisa wenye dhamana kutoka mamlaka tofauti za serikali ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Rais, TAKUKURU, Ofisi ya Mwanansheria Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu.