Waziri Mkuu ataka taarifa ya utendaji kazi ya Mkurugenzi

0
242

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Lindi,- Shaibu Ndemanga, ampelekee taarifa ya utendaji kazi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Waryoba Gunza baada ya Mkurugenzi huyo kushindwa kutoa maelezo kuhusu utekelezaji wa mradi wa maji kwenye kata ya Rutamba.
 
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo wilayani Lindi, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Rutamba akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo na huduma za jamii mkoani Lindi.


 
Amelazimika kutoa agizo hilo baada ya kumtaka Mkurugenzi huyo atoe maelezo ya namna gani alivyojipanga katika kutekeleza mradi wa maji kwenye kata hiyo ambayo wakazi wake wanakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa maji, na kushindwa kutoa maelezo hayo.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa, miradi yote ambayo gharama zake ziko chini ya Shilingi Milioni 100 inatakiwa itekelezwe kwa kutumia fedha za ndani ya halmashauri husika.

“Miundombinu hiyo ilitakiwa iwe imebadilishwa, mradi wa Shilingi Milioni 75 unaomba fedha wizarani ni uvivu,”amesema Waziri Mkuu Majaliwa.