Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua rasmi chaneli mpya ya utalii itakayosaidia kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana nchini.
Akizindua chaneli hiyo katika ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) zilizopo Mikocheni jijini Dar es salaam, Waziri Mkuu Majaliwa amesisitiza mamlaka husika kuongeza juhudi za kutangaza vivutio vya utalii ili Taifa lipate mapato zaidi kutokana na sekta ya utalii.
Amesema kuwa matangazo ya utalii yaliyopo kwa sasa hayatoshelezi kuwashawishi watalii kuja nchini kwa lengo la kuangalia vivutio vya utalii, hivyo ni vema juhudi hizo zikafanyika kwa kushirikisha wadau wote.
Waziri Mkuu Majaliwa ametumia uzinduzi huo wa Chaneli mpya maalumu ya utalii, kutoa wito kwa Watanzania wanaoishi kwenye maeneo mbalimbali ya mapori ya hifadhi kutovamia mapori hayo ili yaendelee kuwa katika hali nzuri na kuvutia watalii wengi zaidi.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, lengo la serikali ni kuongeza idadi ya watalii ifikapo mwaka 2020 na kuboresha maeneo yote yenye vivutio vya utalii ikiwa ni pamoja na barabara za kuelekea kwenye vivutio hivyo.
Akizungumza na wageni mbalimbali waliohudhuria uzinduzi huo wa Chaneli mpya ya Utalii, ameutaka uongozi wa TBC kuipa chaneli hiyo jina la TBC THREE.
Chaneli hiyo ya Utalii imeanzishwa kufuatia wazo lililotolewa na Rais John Magufuli mwezi Mei mwaka 2017 alipozitembelea ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania.
Akitoa wazo hilo, Rais Magufuli alisema kuwa Chaneli hiyo maalumu ya Utalii itasaidia kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini.
Miongoni mwa wadau waliofanikisha uanzishwaji wa Chaneli hiyo mpya ya Utalii ni Shirika la Utangazaji Tanzania, Wizara ya Maliasili na Utalii, wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na wizara ya Mifugo na Uvuvi.