Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakandarasi wa ujenzi wa mradi wa barabara ya mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma kuongeza kasi ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati na kwa viwango.
“Kazi inaendela vizuri, tunataka kazi ikamilike ikiwezekana hata kabla ya muda, Rais Samia Suluhu Hassan anatekeleza miradi hii ili iwanufaishe Watanzania, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunasimamia na inakamilika kwa viwango na wakati”
Amesema hayo leo (Jumapili, Septemba 04, 2022) wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa barabara ya mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma. Mradi huo ni sehemu ya uendelezaji wa jiji hilo.
Pia, Waziri Mkuu amewataka Wahandisi Wasimamizi wa mradi huo wahakikishe wanasimamia kikamilifu wakandarasi ili barabara hiyo iweze kujengwa kwa viwango vilivyokubaliwa kwenye mkataba wa ujenzi wake.
Akizungumza na watanzania walioajiriwa katika mradi huo, Majaliwa amewataka wawe walinzi wa vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi na wahakikishe vifaa vinabaki salama “Pambaneni na wote wenye nia ya kuiba vifaa hivi, tunataka tupate barabara yenye viwango”
Kaimu Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Salome Kabunda amesema kuwa pamoja na mradi huo kusaidia kupunguza msongamano wa magari jiji la Dodoma pindi utakapokamilika, pia umesaidia kutoa ajira kwa wazawa zaidi ya 800.