Waziri Mkuu asisitiza kilimo cha michikichi

0
831

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa vijana mkoani Kigoma kuanzisha mashamba ya michikichi, kwa kuwa zao hilo litawapatia kipato cha uhakika.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo aliposalimiana na Wakazi wa kijiji cha Nyakitondo wilayani Kasulu akiwa njiani kuelekea wilayani  Kibondo kuendelea na ziara yake mkoani humo.

Amewaambia Wakazi hao kuwa serikali imedhamiria kufufua zao la michikichi ili kuliwezesha Taifa kujitosheleza kwenye mafuta ya kula pamoja na kuokoa fedha za kigeni, hivyo ni vema wakachangamkia fursa hiyo.

 “Vijana limeni michikichi, kwani ukipanda ukiwa darasa la tano baada ya miaka mitatu utaanza kuvuna na kujipatia kipato ambacho kitakuwezesha kujikimu”, amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

 Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, kilimo cha zao la michikichi kitawawezesha wananchi hususani vijana kupata mitaji ya uhakika kwa ajili ya shughuli zingine za kiuchumi na kwamba serikali imejipanga kuhakikisha Tanzania inaongoza kwa kilimo cha zao la michikichi katika nchi za Afrika Mashariki.

Wakati huohuo Waziri Mkuu Majaliwa ametembelea kambi ya Wakimbizi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo na kukagua shule ya msingi ya Kassim Majaliwa na baadae wodi ya wazazi katika hospitali Nduta.