Waziri Mkuu aridhishwa na mapambano dhidi ya nzige

0
191

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na kazi ya kupambana na makundi ya nzige yaliyovamia nchini, iliyofanywa na wizara ya Kilimo kwa kushirikiana mashirika mawili ya kupambana na nzige Barani Afrika.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Engaruka wilayani Monduli mkoani Arusha, mara baada ya kukagua shughuli ya udhibiti wa nzige katika kata ya Engaruka.
 
Kazi hiyo inafanywa na Shirika la Kudhibiti Nzige wa Jangwani la Afrika Mashariki pamoja na Shirika la Kudhibiti Nzige Wekundu la Kusini na Kati mwa Afrika.
 
Pamoja na kuridhishwa na kazi hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa ameiagiza wizara ya Kilimo kuweka mikakati ya kukabiliana na makundi ya nzige hao, pindi yatakapoingia tena nchini.
 
“Lazima tuwateketeze, nzige ni hatari na hawapaswi kupewa nafasi hata ya dakika moja kuingia kwenye mashamba yetu, nzige hawa wana uwezo wa kusafiri umbali wa kilomita 200 kwa siku na kuteketeza zaidi ya hekta mbili kwa siku hivyo ni lazima tuwateketeze,” amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema kundi la nzige lililoenda Simanjiro limekwishateketezwa.

Kwa upande wa Siha, Profesa Mkenda amesema nako wameishateketezwa na wilayani Mwanga ambako walikuwa wapite kuelekea Simanjiro nako kwa sasa hakuna nzige.

Amesema wataendelea kufuatilia maeneo ambayo nzige wametua na kuangalia kama wametaga mayai ili wayateketeze. 
 
Nzige walianza kuingia nchini Januari 8 mwaka huu na makundi makubwa yalionekana katika wilaya za Simanjiro kwenye vijiji vya Olchorinyori, Landanai, kitongoji cha Dodoma, Sokoni B na Naberera.

Kwenye wilaya ya Longido nzige walivamia kijiji cha Tingatinga, Nondoto, Orbomba na Komakowa.

Wilaya ya Siha walivamia kijiji cha Namwai na wilaya ya Monduli walivamia vijiji vya Engaruka, Mfereji na Ererendeni.