Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemshukuru Rais John Magufuli kwa kutoa fedha nyingi za kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Ruangwa mkoani Lindi kama ile ya Maji, Elimu, Barabara na Afya.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika mji wa Ruangwa, mkutano ambao pia umehudhuriwa na Rais Magufuli, Waziri Mkuu amesema kuwa, miradi ya Barabara ambayo pia imezinduliwa na Rais Magufuli ni kielelezo cha mapenzi yake kwa Wananchi wa Ruangwa.
Waziri Mkuu Majaliwa amefafanua kuwa, Serikali imetoa fedha kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji wilayani Ruangwa na pia fedha nyingine zaidi ya Shilingi Bilioni 1.5 zimepelekwa kwenye ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo.
Ameitaja miradi mingine kuwa ni ujenzi wa ghala la kuhifadhi mazao mbalimbali, miradi ya umeme vijijini, ujenzi wa chuo cha VETA na ukarabati wa shule za msingi na sekondari.
Halkadhalika, Waziri Mkuu amemshukuru Rais Magufuli kwa kumteua kushika Wadhifa huo na kuahidi kufanya kazi kwa uwezo wake wote ili kuwatumikia Watanzania.