Waziri Mkuu akabidhi magari kwa Polisi Lindi

0
129

Waziri mkuu, Kassim Majaliwa amekabidhi magari mawili kwa ajili ya matumizi ya Jeshi la Polisi mkoa wa Lindi yatakayowezesha askari kutoa huduma katika maeneo ya mkoa huo.

Magari yaliyokabidhiwa ni Toyota Land Cruiser Pickup yenye namba za usajili PT 2615, kwa ajili ya kituo cha polisi cha Mtama na Toyota Land Cruiser V6 lenye namba za usajili PT 4378, kwa ajili ya ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi.

Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kutoa vitendea kazi kwa jeshi la polisi kadiri inavyowezekana ili kuwawezesha askari nchini kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Akizungumza baada ya kupokea magari hayo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, Mtatiro Kitinkwi amesema magari hayo yatawezesha shughuli za doria kufanyika kwa uhakika.

“Magari haya unayotukabidhi yatawezesha shughuli za usafiri wa polisi, doria na usafirishaji wa mahabusu kufanyika kwa uhakika kulingana na jiografia ya halmashauri ya Mtama,” amesema.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye kwa niaba ya wananchi ameishukuru Serikali kwa kutoa magari hayo ambayo yatawezesha shughuli za ulinzi na usalama katika jimbo hilo na mkoa kufanyika kwa ufanisi zaidi.