Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza mawaziri kukaa na wakandarasi na kutathmini umalizaji wa ujenzi wa majengo ya serikali mkoani Dodoma.
Waziri Mkuu Majaliwa amekutana na Mawaziri na Makatibu Wakuu na kuwataka wafike kwenye maeneo ya ujenzi wa ofisi zao, kutathmini uwezo wa wakandarasi wanaojenga majengo ya wizara na kama wakandarasi hao hawana uwezo wa kumaliza ujenzi huo wabadilishwe mara moja.
Agizo hilo amelitoa leo alipofanya ziara ya kujionea ujenzi unavyoendelea na kusema endapo wakandarasi hao hawatakuwa na uwezo mkubwa lazima wabadilishwe.
“Mawaziri mliopo na makatibu wakuu wote kaeni na wakandarasi wenu hapa site ili waeleze kazi hii itakamilishwa lini lengo letu ni kuhakikisha kuwa kazi hii inakamilishwa kwa wakati,”alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Amewataka wakandarasi wahakikishe wanaongeza idadi ya vibarua ili kazi hiyo iweze kwenda haraka na kuipongeza Wizara iliyofanya vizuri kuliko zote ni ya Utumishi, ambao katika ujenzi wao ofisi zao uko katika hatua nzuri.
Katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amemweleza Waziri Mkuu kwamba kuna wagongaji wa kokoto ambao wamepokea fedha lakini wakaamua kufunga machimbo yao kwa sababu ya sikukuu.
