Waziri Mkuu aagiza sekondari ya Tunduru ipelekewe gari

0
191

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amempa muda wa siku mbili Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, – Gaspar Balyomi awe amepeleka gari katika shule ya sekondari Tunduru kwa ajili ya kuwahudumia Walimu na Wanafunzi shuleni hapo.
 
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa muda huo alipokuwa akikagua ukarabati wa shule ya sekondari Tunduru ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Ruvuma.

Ametoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Tunduru Kusini, Daimu Mpakate kumueleza kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya usafiri.
 
“Mkurungezi Jumatatu lete gari moja hapa likiwa limeandikwa Shule ya Sekondari Tunduru lije kutoa huduma kwa watoto na walimu wetu, hii shule ina Wanafunzi zaidi ya 600 na walimu 28 lazima iwe na usafiri ambao hata mtoto akiugua afikishwe hospitali,” ameagiza Waziri Mkuu Majaliwa.
 
Kuhusu ukarabati uliofanyika shuleni hapo, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na ametumia fursa hiyo kumpomgeza Mkuu wa Shule, Mwalimu Amini Limia pamoja na kamati ya ujenzi kwa kazi nzuri ya usimamizi waliyoifanya.
 
Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya Tano ilipoingia madarakani ilianzisha mkakati wa kukarabati shule zote kongwe nchini ikiwemo shule ya sekondari ya Tunduru ambayo ukarabati wake umegharimu zaidi shilingi milioni 700.

Mkoa wa Ruvuma umepewa jumla ya shilingi bilioni 3.7 kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe za sekondari ikiwemo hiyo ya Tunduru.