Waziri Makamba atoa agizo TPDC, PURA

0
62

Waziri wa Nishati, January Makamba ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), kuhakikisha mradi wa uchimbaji gesi kitalu cha Ruvuma na Mtwara unamalizika kwa wakati ili kuipatia serikali mapato, tozo na gawio kubwa.

Makamba ametoa agizo hilo mkoani Dar es Salaam wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa nyongeza wa Uzalishaji na Ugawanaji Mapato (PSA), kitalu cha Ruvuma – Mtwara kati ya TPDC na kampuni za ARA Petroleum na Ndovu Resources.

Amesema dhamira ya serikali ni kuona mradi huo unakamilika ndani ya kipindi cha miezi 12 hadi miezi 18 na kuanza kuzalisha gesi na kuongeza kuwa hategemei kusikia unachelewa kutokana na kukosa fedha.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa ya Kusini, mkuu wa mkoa wa Lindi, Zainab Telack ameishukuru serikali kwa kuwapatia mradi huo.

Amesema wananchi wa mikoa ya Kusini watanufaika wakati wa ujenzi wa mradi huo ikiwa ni pamoja kupata ajira wakati wa ujenzi wake.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu TPDC Dkt. James Mataragio amesema, utafiti umeshafanyika na kinachoendelea hivi sasa ni uchimbaji wa visima na kuanza uzalishaji wa gesi ambayo itakuwa msaada mkubwa katika uanzishwaji wa viwanda vya mbolea.

Amesema tayari hatua za awali za kuchimba bomba katika mradi huo wa uchimbaji gesi kitalu cha Ruvuma na Mtwara zimeanza kwenye kijiji cha Ntory kuelekea Madimba kwa ajili ya kuichakata, ambapo inatatajiwa kuzalishwa kiwango cha futi za ujazo trilioni 1.6.