Waziri Lukuvi awashukia viongozi wapora ardhi

0
342

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amekerwa na tabia ya baadhi ya viongozi kuhusika kupora ardhi ya wananchi na kueleza kuwa muarobaini wa viongozi hao umefika kufuatia watendaji wa sekta ya ardhi kuhamishiwa Wizarani sambamba na kuanzishwa ofisi za ardhi katika mikoa.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema hayo wakati wa kuzindua ofisi ya ardhi mkoani Katavi jana ikiwa ni mfululizo wa uzinduzi wa ofisi za ardhi kwenye mikoa mbalimbali nchini.

Alisema, wapo baadhi ya viongozi wa wilaya na mkoa ambao ni sehemu ya migogoro ya ardhi na wamekuwa wakitumia madaraka yao vibaya kwa kupora na kuuza ardhi za wananchi tabia aliyoieleza kuwa inamkera Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli.

Kwa mujibu wa Lukuvi, uanzishwaji ofisi za ardhi za mikoa pamoja na uhamishaji watendaji wa sekta ya ardhi kutoka TAMISEMI kuja Wizarani unatoa nguvu kwa watumishi wa sekta ya ardhi kutumia na kusimamia sheria na kuonya viongozi kutojihusisha na kupora ardhi za wananchi na kubainisha kuwa ardhi itapangwa na kusimamiwa kwa mujibu wa sheria.

“Kuna viongozi wa kuchaguliwa na wa kuteuliwa wanaotumia madaraka yao vibaya kwa kupora ardhi za wananchi, safari hii hakuna fursa maana watendaji wote wa sekta ya ardhi wako chini ya Wizara ya ardhi, madiwani hawawezi tena kuwaazimia kuwafukuza”, alisema Lukuvi

Akizungumzia suala la upimaji ardhi katika Mkoa wa Katavi, Lukuvi aliagiza hadi kufikia mwisho wa mwaka huu 2020 vijiji vyote katika mkoa huo viwe vimepimwa na kupatiwa hati za kijiji sambamba na wamiliki 15,000 waliokwama kupewa hati kutokana na urasimu kupatiwa hati zao na kuweka wazi kuwa, hivi sasa hakuna visingizio kwa kuwa vifaa kwa ajili ya upimaji vipo.

Agizo la Lukuvi linafuatia kuelezwa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Katavi, Siyabumi Mwaipopo kuwa kati ya vijiji 172 vilivyopo kwenye mkoa huo ni vijiji vitatu tu ndivyo vilivyopimwa na kupatiwa hati za vijiji.

“Mwaka huu uwe wa mwisho kwa migogoro ya ardhi nchini kwani nyenzo zote zipo ikiwemo wataalamu pamoja na vifaa vya upimaji na nawataka viongozi wa wilaya na mkoa wasiwe sehemu ya migogoro”, alisema Lukuvi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula alisisitizia suala la ukusanyaji maduhuli ya Serikali kupitia kodi ya pango la ardhi ambapo alisema ni muhimu wamiliki wa ardhi wakaepuka kuwa na malimbikizo ya kodi ya ardhi kwa kutii sheria ya kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera mbali na kushukuru uamuzi wa kuanzisha ofisi ya ardhi katika mkoa wake, aliwataka wananchi wa Katavi kuitumia fursa ya kuwa na ofisi ya ardhi ya mkoa kupima ardhi na kumilikishwa na kusisitiza kuwa mkoa wake utaandaa opresheni maalum ya kupima ardhi katika mkoa mzima.

Uzinduzi ofisi ya ardhi mkoa wa Katavi uliambatana na makabidhiano ya vifaa mbalimbali ambapo Waziri Lukuvi alikabidhi gari lenye thamani ya shilingi milioni 150 pamoja na vifaa vya upimaji kwa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi wa sekta ya ardhi kwenye halmashauri hiyo.