Waziri Lukuvi awapigia simu walioshindwa kuchukua hati zao za ardhi

0
181

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewaagiza Wamiliki wote wa ardhi nchini waliofanya taratibu za kupata hati kufika katika ofisi za ardhi za mikoa kuchukua hati zao ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Waziri Lukuvi ametoa agizo hilo kufuatia kuwepo kwa hati 20,752 ambazo hazijachukuliwa katika ofisi za ardhi kwenye mikoa 26 ya Tanzania Bara, na hivyo kufanya kuwepo mlundikano wa hati katika ofisi za Wasajili wa Hati Wasaidizi kwenye Ofisi za Ardhi za mikoa.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Lukuvi ameanza kazi ya kuwatafuta wamiliki wa ardhi walioshindwa kuchukua hati zao kwa kuwapigia simu na kuwataka wazifuate hati hizo.

Miongoni mwa wamiliki wa ardhi jijini Dar es salaam waliopigiwa simu ili kufuata hati zao ni kutoka maeneo ya Salasala, Kibada na Mbezi Msakuzi ambapo baadhi yao walionesha kushangazwa na uamuzi wa Waziri Lukuvi wa kuwapigia simu.

Mkoa wa Dar es salaam ndio unaoongoza kwa wamiliki wake wa ardhi kutochukua hati zao ukifuatiwa na mkoa wa Pwani.