Waziri Jafo ‘amkaba’ mfanyabiashara aliyetelekeza makontena bandarini

0
160

Na,Emmanuel Samwel TBC

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo ameagiza kukamatwa kwa Kaissy Mkurugenzi wa Kampuni ya Seif for Tobacco Trading Co. Ltd aliyeingiza nchini makontena zaidi ya mia tano (500) yenye malighafi ya Molasesi iliyoharibika na kuyatelekeza katika Bandari ya Dar es Salaam.

Waziri Jafo ameagiza hayo hii leo mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na kueleza kuwa kamwe Tanzania haiwezi kugeuzwa kuwa dampo kwa kuruhusu bidhaa kutoka nje ya nchi ambazo muda wake wa matumizi umeisha kuingizwa nchini kwa lengo la kutupwa kiholela.

“Ndugu zangu katika kusimamia mazingira hatuna mzaha, afya za binadamu na mimea ni dhamana yetu, sitaruhusu afya za watanzania kuwekwa rehani” Jafo alisisitiza.

Aidha Waziri Jafo ametoa siku kumi kwa watu wenye mizigizo iliyoisha muda wake ikiwemo mbolea na kemikali zingine kujisalimisha wenyewe kabla heria haijachukua mkondo wake huku akigiza Baraza la uhifadhi na usimamizi wa Mazingira NEMC kuanza ukaguzi mara moja katika bandari kavu ili kubaini uwepo wa mizigo mingine kama hiyo.

Imebainika kuwa mfanyabiashara huyo aliyetambulika kwa jina moja tu la Bw. Kaissy aliingia nchini kwa hati ya utembezi (tourist) na baadae kupatiwa kibali cha uwekezaji kupitia Export Processing Zone (EPZA) kilichomruhusu kuwekeza katika uzalishaji wa shisha kibali ambacho kilifutwa baada ya kugundulika kuwa kuna udanganyifu mkubwa kuhusu uwekezaji wake.