Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewasimamisha kazi watumishi sita akiwemo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA), Tamimu Katakwemba pamoja na Afisa Maji Bonde la Wami-Ruvu, Simon Ngonyani kwa tuhuma mbalimbali za matumizi mabaya ya ofisi.
Akizungumza na watumishi wa MORUWASA na ofisi ya maji bonde la Wami Ruvu mjini Morogoro, Waziri Aweso amesema Katakwemba amesimamishwa kazi kwa kosa la kusaini mkataba wa Euro milioni 70 kwa ajili ya upanuzi wa Bwawa la Maji la Miundu bila ridhaa ya wizara ya maji.
Kwa upande wa afisa wa maji bonde la Wami Ruvu, Aweso amesema amemsimamisha afisa huyo kwa kushindwa kuwajibika kusimamia miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali pamoja na kushindwa kuwasimamia watumishi wake.
Wakati huo huo amewasimamisha kazi watumishi wanne wa MORUWASA kwa kuiuka maadili ya utumishi wa umma.