Waziri aagiza daktari kusimamishwa kazi kwa kutoa taarifa zisizo sahihi

0
421

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima ameagiza kusimamishwa kazi Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chunya, Dkt. Felista Kisandu kupisha uchunguzi kwa madai ya kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa ajabu katika Kata ya Ifumbo, Mbeya.

Katika taarifa yake, Waziri Gwajima amesema kuwa Dkt. Kisandu amekiuka mwongozo wa utoaji wa taarifa za milipuko ya magonjwa kama ilivyoelezwa kwenye Sheria ya Afya ya Umma (Public Health Act) ya mwaka 2009 ambayo inataka mamlaka kwa kupitia waziri kutoa taarifa endapo kuna janga la kiafya.

Dkt. Gwajima amesama, “Ninaagiza mamlaka ya ajira ya Dkt. Felista Kisandu ambaye ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chunya ichukue hatua za kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi chini ya Baraza la Madaktari na taarifa nipate ndani ya siku 10.”

Waziri ameeleza kuwa Dkt. Kisandu alikiri kuwepo kwa ugonjwa huo katika Wilaya ya Ifumbo pasi na kujiridhisha kuhusu taarifa za ugonjwa unaodaiwa kuwafanya watu kutapika damu, kwa maelezo kuwa amepata taarifa kutoka kwa wananchi na diwani.

Timu ya wataalamu iliyotumwa eneo hilo imebaini kuwa si kweli kwamba kuna ugonjwa huo, na pia taarifa kwamba kuna watu 15 wamefariki kwa pamoja sio za kweli.