Wazazi wajitolea kujenga sekondari ya kijiji

0
191

Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika kijiji cha Chekereni Weruweru wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, wataondokana na adha ya kutembea umbali wa kilomita 34 kwenda shule ya sekondari ya TPC baada ya wazazi wa kijiji hicho kuanza ujenzi wa shule ya sekondari ya kijiji.

Baadhi ya Wazazi kijijini hapo wamedai kuwa, wamekuwa wakishindwa kumudu gharama za usafiri kila siku kwa watoto wao kutokana na umbali uliopo kutoka kijiji cha Chekereni Weruweru hadi ilipo shule hiyo ya sekondari.

Wamesema umbali wa kwenda shule ya sekondari ya TPC umekuwa ukihatarisha usalama wa watoto wao, hivyo ujenzi wa shule hiyo utakapokamilika utawasaidia Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kusoma eneo la karibu.

Akizindua ujenzi wa shule hiyo, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Moshi, – Morris Makoi ameiagiza Idara ya Elimu ya Sekondari ya wilaya hiyo kukamilisha usajili wa shule hiyo mapema ili kuwezesha wanafunzi kuanza masomo mwezi Aprili mwaka huu.

Tayari shilingi milioni 28 zimepatikana kwa ajili ya kuanza ujenzi wa shule hiyo ya sekondari katika kijiji cha Chekereni Weruweru.

Ujenzi wa kila darasa utagharimu shilingi milioni Saba, na lengo la wazazi hao ni kuanza na ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa.