Wazazi simamieni watoto wanavyotumia simu

0
175

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawasimamia vyema watoto wao katika matumizi sahihi ya simu ili yaendane na madhumuni yaliyokusudiwa kwenye teknolojia.

Rais Samia amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Skuli ya Msingi ya Mwanakwerekwe iliyojengwa kwa Fedha za UVIKO19 ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambapo amesema ni vyema wazazi na walezi kuwaunganisha watoto wao na kiungio (link) cha Wizara ya Elimu chenye mambo muhimu ya kujifunza kuhusiana masuala ya elimu.

“Watoto wetu wanachezea sana simu hivyo wazazi tujitahidi kuwaelekeza watoto kutumia simu kwa mambo ya muhimu na sio kuingia kwenye YouTube kutazama na kusikiliza taarabu huku mzazi ukiwa huna habari badala ya kusoma mambo ya msingi,” amesema Dkt. Samia.

Pia, amesisitiza kuwa ni vyema waanze kufundishwa masomo ya sayansi wakiwa bado wadogo ili waweze kufanya vizuri siku za usoni kwenye masomo ya sayansi tofauti na hali ilivyo hivi sasa.

“Nimeona nia njema ya serikali kwamba watoto sasa lazima watumie teknolojia lakini pia lazima waanze kusoma masomo ya sayansi mapema, wataweza kufanya vizuri siku za usoni,” amesema.

Aidha, Rais Samia amegusia suala la mitaala kuwa ni eneo mojawapo linalohitaji kubadilishwa ili kuwasaidia vijana kuwa na mwelekeo unaoeleweka kwenye taaluma yao baada ya masomo.