Watu wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka sita likiwemo kosa la uhujumu na kuisababisha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hasara ya zaidi ya shilingi milioni 200.
Washitakiwa hao Mhandisi Baraka Mtunga, mkazi wa Mbezi Beach na mfanyabiashara Rajab Katunda, mkazi wa Mikocheni B jijini Dar es Salaam wadaiwa kutenda makosa hayo katika maeneo tofauti ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Sadaan mkoani Pwani na Dar es Salaam kati ya Decemba 13, 2019 na Septemba 28, 2020.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Kassian Majaliwa amedai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Decemba 13, 2019 na Septemba 28, 2020 katika hifadhi hiyo na Dar es Salaam washitakiwa hao walikula njama ya kuongoza genge la uhalifu kunyume na sheria.
Aidha katika shitaka lingine amedai washitakiwa hao katika tarehe tofauti na maeneo tofauti ya hifadhi ya Sadaan washitakiwa hao walisimika vifaa vya mawasiliano katika hifadhi hiyo huku wakijua kufanya hivyo ni kosa.
Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusililiza mashitaka ya uhujumu uchumi.
Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 82 ya mwaka 2020 imeahirishwa hadi Oktoba 27 mwaka huu itakapotajwa na washitakiwa wote wamepelekwa rumande, baada upande wa mashitaka kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.