Wawekezaji kutoka Vietnam wakaribishwa nchini

0
434

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, Trinh Dinh Dung na kuwakaribisha wawekezaji kutoka Vietnam kuja kuwekeza hapa nchini.

Amesema anatambua kwamba Vietnam inafanya vema katika suala la mazao ya kilimo kwa kuongeza tija kwenye mazao hayo na kukifanya kilimo kuwa cha biashara, hivyo amezialika kampuni za Vietnam kushirikiana na Tanzania katika mikakati yake ya kuendeleza kilimo.

Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati wa mkutano wake na Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, ambapo ametumia fursa hiyo kumhakikishia kwamba Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano wake na Vietnam kwa manufaa ya watu wa nchi mbili hizo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, Trinh Dinh Dung ameishukuru serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na kwamba ameomba ushirikiano huo uimarishwe kupitia ziara za viongozi wakuu wa nchi mbili hizo.

Naibu Waziri Mkuu huyo wa Vietnam, amemhakikishia Waziri Mkuu kwamba Serikali ya nchi hiyo itaimarisha ushirikiano wake na serikali ya Tanzania hususani katika sekta za kilimo, biashara na uvuvi.